Kigoma, Katavi na Rukwa zanufaika na vifaa tiba kutoka Ujerumani

 

Taasisi ya huduma za macho ya Ujerumani inayofahamika kama Tanzaneye imetoa misaada ya vifaa tiba, majengo na mafunzo ya tiba ya macho wenye thamani ya Zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa nchini Tanzania. Mwandishi wetu Prosper Kwigize ametuandalia ripoti ifuatayo

Akitoa taarifa katika hafla ya kukabidhi vifaa tiba na uzinduzi wa ujenzi wa kituo kikubwa cha tiba ya Macho katika hospitali ya Kabanga inayomilikiwa na Jimbo Katoliki la Kigoma, Mkurugenzi wa Tanzaneye kutoka Bonn Ujerumani Dr. Karsten Paust amesema, taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2017 inalenga kuunga mkono serikali na kanisa katoliki katika kutoa huduma ya macho katika maeneo ambayo hayajafikiwa na taasisi nyingine

Askofu Joseph Mlola na Elisante Mbwilo wakionesha moja ya kifaa tiba cha macho kilichokabidhiwa na Dkt. Karsten Paust (katikati) kutoka taasisi ya TanzanEye ya Ujerumani

Paust amebainisha kuwa lengo la shirika hilo linaloundwa na wajerumani na watanzania ni kusaidia nchi ya Tanzania kuongeza idadi ya wataalamu wa afya ya macho kwa kutoa mafunzo ambapo tayari madaktari 45 wamejengewa uwezo

Akipokea misaada hiyo, Askofu wa jimbo katoliki la Kigoma Joseph Mlola ameishukuru Tanzaneye kwa kukubali kushirikiana na kanisa kuokoa afya ya macho kwa wananchi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika na kuahidi kuimarisha ushirikiano baina yao.

Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma Dkt. Ibrahim Sahele amekiri kuwa mkoa huo una upungufu mkubwa wa vifaa tib ana wataalamu wa huduma ya afya ya macho na kwamba ufadhili iliotolewa na tanzaneye umekuja kwa wakati sahihi

Dkt Salehe anabainisha kuwa mkoa wa Kigoma pekee una vituo vya kutolea huduma za afya Zaidi ya 300 vinavyokabiliwa na uhaba wa vifaa tiba ya macho sambamba na miundombinu na anatoa wito kwa wadaua Zaidi kujitokea kusaidia sekta hiyo

Dkt. Karsten Paust mkurugenzi wa TanzanEye akisikiliza kwa umakini maelezo ya wadau wa afya baada ya kukabidhi vifaa vya tiba ya macho katika Hospitali ya Rufaa ya Kabanga mjini Kasulu inayomilikiwa na Kanisa Katoliki

Akizungumza kuhusu takwimu, Mratibu wa TanzanEye nchini Tanzania Bw. Ryner Linuma anaeleza kuwa kiwango cha magonjwa ya macho nchini Tanzania kinafikia asilimia 4 ya wagonjwa wote na kwamba juhudi mbalimbali zinahitajika ili kuondoa uwezekano wa wagonjwa kupata upofu

Linuma anabainisha kuwa changamoto kubwa ya macho nchini Tanzania ni tatizo la mtoto wa jicho ambalo linafikia asilimia 70 ya magonjwa yote ya macho nchini Tanzania

Akihutubia katika hafla hiyo kaimu Katibu tawala wa mkoa wa Kigoma Bw. Elisante Mbilo amekiri kuwa serikali inahitaji wadau Zaidi katika kuboresha huduma za afya hasa katika maeneo ya vijijini

Picha ya pamoja ya viongozi wa Kanisa, TanzanEye, Serikali na wataalamu wa afya wa hospitali ya rufaa Kabanga. kutoka kushoto ni Mwl. Vumilia Simbeye mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kasulu, Karsten Paust kutoka TanzanEye, Elisante Mbwilo kaimu RAS, Askofu Joseph Mlola na padre wa kanisa katoliki Parokia ya Kabanga.

Jumla ya vituo vya huduma za afya ya macho 18 ikiwemo hospitali za halmashauri za wilaya ya Kakonko, Kibondo, Uvinza, Buhigwe, Kasulu na Halmashauri ya Mji wa Kasulu zimepata msaada wa vifaa tiba ya macho kutoka TanzanEye ya Ujerumani

 

 

 

Post a Comment

0 Comments