Dunia leo inaadhimisha siku ya
wakimbizi kimataifa huku kukiwa na wimbi jipya la wakimbizi wapya katika maeneo
mbalimbali kutokana na kuwepo kwa mapigano katika nchi ya DRC, na nchi za
Mashariki ya Kati hususani Israel, Palestina, Yemen, Ukraine, Urusi na Irani.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa
yanayohifadhi wakimbizi wa zamani wa DRC na Burundi na kundi jipya la wakimbizi
kutoka Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Tofauti na miaka ya nyuma ambapo
maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yaligubikwa na malalamiko mengi, mwaka
huu wakimbizi, UHNCR na jamii wameungana kushukuru namna Tanzania na watanzania
wanavyovumiliana na kushirikiana katika kuhakikisha kunakuwepo na mahusiano
mazuri, utu, amani na mshikamano miongoni mwa raia na wakimbizi.
Akihutubia katika mkutano mkubwa wa
wakimbizi mapema leo katika kambi ya Nyarugusu inayohifadhi Raia wa Burundi
pamoja na DRC, Mkuu wa ofisi ys UNHCR Bw. Jean Bosco Ngomoni ameishukuru
Tanzania na raia wake kwa kuonesha mshikamano thabiti kwa wakimbizi.
Bw. Ngomoni amesema hatua
mbalimbali za utoaji wa huduma zinaendelea kutekelezwa sambamba na kuhakikisha
kuna amani ya kudumu katika nchi walizotoka na akasisitiza kuwa nchi ya Burundi
sasa ina amani na usalama wa uhakika unaowezesha wakimbizi kurejea nchini mwao
kwa hiari ili wakaijenge nchi yao tofauti na DRC ambako hali bado haijaimarika.
Mkuu huyo wa UNHCR Kasulu amesisitiza
kuwa kutokana na mshikamano wa pamoja na serikali na umoja wa mataifa, Tanzania
imeendelea kupokea wakimbizi wapya na kwamba mwaka 2023 wakimbizi takribani
14,000 waliingia nchini humo na wengine 3000 wamepokelewa mwaka huu wakitokea
nchi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na kwamba serikali ya Tanzania imekuwa
mstari wa mbele kuhudumia wakimbizi wanaoingia nchini na kusisitiza kuwa
wakimbizi watakakaofanya maamuzi ya kurejea nchini mwao watakuwa wamefanya
maamuzi sahihi.
Wakimbizi wenyewe wana maoni gani
kuhusu siku ya mkimbizi duniani? Hawa hapa ni baadhi ya waliozungumza na vyombo
vya habari na kukiri kuwa Tanzania imekuwa sehemu ya msaada kwa usalama wa
maisha yao, na kupongeza serikali inayoshirikiana na Umoja wa Mataifa kutoa
huduma kwa wakimbizi ingawa kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa
misaada hususani chakula. Ilakoze Lyidia, ni mama mkimbizi kutoka nchi ya
Burundi mwenye
Naye Amrani Juma, kutoka nchi ya
DRC ambaye yupo kambini tangu mwaka 1998 anakiri kuwa kuna hali mbaya ya uchumi
inayoikumba dunia kutokana vita vinavyoendelea imekuwa kikwazo kwa upatikanaji
wa huduma muhimu zikiwemo za afya na elimu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kambi
kambi ya Nyarugusu Bw. Manilakiza Japhet, alisema bado zipo changamoto
zinazowakabili wakambizi wanaoishi kambini na kuomba UNHCR kwa kushirikiana na
serikali ya Tanzania na mataifa yanayotoa huduma kambini humo kutafuta hifadhi
za kudumu kwaajili ya wakimbizi hao pamoja na nchi ya Tanzania kutoa hifadhi ya
kudumu.
Misimamo ya Rais wa Marekani Donald
Trump kuhusu wahamiaji, nayo imegusa siku ya wakimbizi ambapo pamoja na
kulaumiwa kwa kuzuia fursa kwa wakimbizi kupata hifadhi nchi ya tatu, jumuiya
ya wakimbizi nchini Tanzania inauomba umoja wa mataifa kutafuta nchi nyingine
tofauti na Marekani kama anavyosisitiza Mwenyekiti wa kambi
Wakati huo huo Wakimbizi katika
kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuwalea
watoto katika maadili yanayofaa ili kizazi chao kiweze kumaliza tatizo la
ukimbizi linalozikumba baadhi ya nchi za maziwa makuu.
Akizungumza katika maadhimisho hayo
Mkuu wa kambi ya Nyarugusu Bw. Siasa Majenje amesema kutokuwa na malezi bora
kumetajwa kuwa tishio kwa vizazi vilivyopita na vilivyopo na kusisitiza malezi
bora kuwa ni suluhu la kudumu kwa ukimbizi.
"Vurugu zinazotokana na vita
katika maziwa makuu zimekuwa zikizalisha wakimbizi wengi ambapo wanaoteseka zaidi
ni watoto, naomba muwalinde na kuwalea watoto wenu vizuri ili kuokoa maisha
yao, huenda kesho wakawa sababu ya kusitisha mapigano" Anasema Majenje
Mkuu huyo wa kambi alisema vurugu
nyingi zinasababishwa na madhaifu ya kibinadamu ya kutamani mali na madaraka na
kwamba hali hiyo inaweza kubadilika kwa kupanda mbegu za amani kwa watoto ili
watakapokua wasifanye makosa kama waliyoyafanya wazazi wao.
Kuhusu maombi yaliyowasilishwa na
wakimbizi, Mkuu huyo wa kambi ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi ameahidi
kuyawasilisha kwa mamlaka zinazohusika ili yafanyiwe kazi na kutafutiwa
ufumbuzi
Tazama Video namna wakimbizi walivyoonesha vipaji vya hali ya juu katika michezo mbalimbali kwa kubofya link hii https://www.youtube.com/shorts/gI2DhW-FyVo?feature=share
Pamoja na hotuba, ngoma na burudani nyingine kumefanyika mchezo wa kirafiki wa mpira wa miguu uliokutanisha timu ya wakimbizi na timu ya raia kutoka Makere halmashauri ya wilaya ya Kasulu
Katika mchezo huo wa ujirani mwema, kikosi cha wakimbizi kimeondoka kifua mbele kwa ushindi wa magoli matatu (3) kwa nunge shidi ya Makere FM
Mshindi wa kwanza amekabidhiwa kombe pamoja na mbuzi watatu (3) wakati Makere FC ikipata zawadi ya Mbuzi wawili (2).
Akikabidhi zawadi hizo Mkuu wa Kambi hiyo Bw. Manjenje amewapongeza kwa mchezo mzuri unaodhihirisha ujirani mwema baina ya Wakimbizi na Wenyeji.
0 Comments