Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima akizungumza wakati akitangaza ratiba na orodha ya vyama ambavyo wagombea wake wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watafika katika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma kuchukua fomu za utezi kwaajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Kailima amesema hadi kufikia leo Agosti 08, 2025 vyama 14 vimeijulisha Tume ratiba ya wagombea wa vyama husika kuchukua fomu. Zoezi hilo litaanza Agosti 09 hadi 27 mwaka huu na vyama vingine vitakavyojitokeza vitapangiwa ratiba.
*****************
Na Mwandishi Wetu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza ratiba ya kuchukua fomu za uteuzi kwa wagombea wa vyama 14 vya siasa waliopendekezwa kugombea nafasi za Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaanza kesho tarehe 09 Agosti, 2025.
Mkurugenzi wa INEC, Ndugu,
Kailima Ramadhani akizungumza jijini Dodoma leo tarehe 08 Agosti, 2025 amewataja
wagombea watakaochukua fomu kesho tarehe 09 Agosti, 2025 kuwa ni kutoka Chama
cha Mapinduzi (CCM), National Reconstruction Alliance (NRA) na Alliance for
African Farmers Party (AAFP).
“Hadi leo tarehe 08 Agosti,
2025, tumepokea barua kutoka katika vyama vya siasa kumi na nne (14) zikiainisha
tarehe na muda ambao wanachama wa vyama vyao waliowapendekeza kugombea nafasi
za Kiti cha Rais na Makamu wa Rais watafika ofisi za Tume zilizopo Njedengwa
Jijini Dodoma kwa ajili ya kuchukua Fomu za Uteuzi,” amesema Ndugu. Kailima.
Amevitaja vyama vingine na
tarehe za wagombea kuchukua fomu kuwa ni pamoja na na Chama cha MAKINI tarehe 10
Agosti, 2025, The National League for Democracy (NLD) tarehe 10 Agosti, 2025,
United Peoples’ Democratic Party (UPDP) tarehe 10 Agosti, 2025 na African
Democratic Alliance Party (ADA – TADEA) tarehe 11 Agosti, 2025.
Vyama vingine ni Union for
Multiparty Democracy (UMD) tarehe 11 Agosti, 2025, Tanzania Labour Party (TLP)
tarehe 11 Agosti, 2025, Chama Cha Kijamii (CCK), tarehe 12 Agosti, 2025, Chama
cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), tarehe 12 Agosti, 2025, Alliance for Democratic
Change (ADC), tarehe 12 Agosti, 2025, Democratic Party (DP) tarehe 13 Agosti,
2025 na National Convention for Construction and Reform (NCCR – MAGEUZI) tarehe
15 Agosti, 2025.
Ndugu Kailima amesema tayari Tume
imeviandikia vyama hivyo vya siasa barua kuvijulisha kuhusu ratiba hiyo ya
utoaji fomu za uteuzi.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza ratiba ya kuchukua fomu za uteuzi kwa wagombea wa vyama 14 vya siasa waliopendekezwa kugombea nafasi za Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaanza kesho tarehe 09 Agosti, 2025.
“Aidha, ni muhimu tukumbuke kuwa, ratiba hii inahusu vyama kumi na nne (14) pekee vilivyowasilisha taarifa hadi kufikia leo tarehe 08 Agosti, 2025, hivyo iwapo vyama vingine vitajitokeza, tutaandaa ratiba husika na kuwajulisha,” amesema.
Amevipongeza vyama vyote vya siasa kwa kuendelea kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 na kuongeza kuwa, Tume kwa upande wake itazingatia katiba, sheria na kanuni wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
0 Comments