Rais Dr. Samia aweka historia Pangani Tanga



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja la Mto Pangani na Barabara ya Bagamoyo (Makurunge) – Saadani na Tanga – Pangani yenye urefu wa kilomita 256.

Rais Dkt. Samia amesema barabara hiyo inayounganisha Mikoa ya Pwani na Tanga kupitia Pangani inaenda kufungua fursa nyingi za kiuchumi, kiutalii na kibiashara katika maeneo yanayopitiwa na barabara hiyo.

Zoezi hilo limefanyika leo katika Wilaya ya Pangani ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkoa wa Tanga.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa barabara hiyo itaunganishwa na shoroba nyingine za maendeleo ikiwemo Eneo la Maalum la Kiuchumi na Bandari Kubwa ya Kisasa itakayojengwa katika Wilaya ya Bagamoyo, hali itakayochochea fursa zaidi za kiuchumi kwa Watanzania.

Mradi huo wa ujenzi wa Daraja la Mto Pangani na Barabara ya Bagamoyo hadi Tanga umenufaika na ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika katika kuunga mkono lengo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuboresha miundombinu na usafiri nchini na kuchochea fursa mbalimbali za kiuchumi na uzalishaji.

Katika hatua nyingine, leo Rais Dkt. Samia amegawa boti za uvuvi 35 na boti saidizi 60 kwa wavuvi wa Pangani kwa mkopo ili kuimarisha shughuli za uvuvi katika Wilaya hiyo. Boti hizo zenye uwezo wa kubeba tani 3 hadi 5 za samaki ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuwakopesha wavuvi boti 120 na boti saidizi 118 nchi nzima.

Akizingumzia zoezi hilo Rais Dkt. Samia amewarai wanufaika wa boti hizo za uvuvi kuzitunza, kuzifanyia kazi na kulipa mikopo husika ili wananchi katika maeneo mengine waweze kunufaika na mpango huo wa ugawaji wa boti za uvuvi.

Akizungumza baada ya kuweka Jiwe la Msingi katika Msikiti wa Ijumaa unaojengwa na waumini wa dini ya Kiislam katika Jiji la Tanga, Rais Dkt. Samia pia ametoa rai kwa viongozi wa dini na wananchi kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya yanayoathiri vijana na maendeleo ya jamii.


Post a Comment

0 Comments